Friday, 6 April 2012






MRADI WA KUPANDA MIKOKO WAGEUZA MAISHA YA WAKAZI.
.
Unapofika katika ufuo wa bahari wa Kidongo viungani mwa kijiji cha Majaoni katika kaunti ya Mombasa, utakumbana na utulivu mkuu. Miti ya mikoko iliyochanwa vizuri inatoa taaswira ya mandhari ya kupendeza kwa kila anayefika hapa. Kuna misitu kadhaa ya mikoko hapa, jambo ambalo linaashiria utunzaji mzuri wa mti huu ambao unakumbwa na hofu ya kumalizwa kutokana na kukatwa kiholela.
Wakati mwandishi huyu alipotembelea ufuo huu hivi majuzi, ilidhihirika kwamba hizi zimekuwa juhudi kubwa za wakazi wenyewe hapa wakitaka kuona mti wa mkoko unahifadhiwa vyema na katika mazingira salama.  Upekuzi wangu ukadhihirisha kwamba hizi ni juhudi ambazo zimekuwa zikitekelezwa na kikundi cha Kidongo Beach Management Unit, mpango wa wakazi ambao unasimamia upanzi wa mikoko katika umbali wa kilomita kumi.
Kulingana na mwenyekiti wa mradi huu Bw Kokota Chivatsi,mradi huu umekuwa na manufaa kwa wakazi ambao wamekuwa wakimiminika hapa kupanda mikoko kwa ajili ya kutunza mazingira.
“Mradi huu tulianzisha mwaka wa 2006. Tulikuwa wanachama wachache lakini kadri mradi ulivyozidi kupanuka ndipo tulipoendelea kupata wanachama wengi,” akasema mwenyekiti huyo.
Kulingana na Bw Chivatsi, mradi huu sasa umeanza kupata sifa kutokana na juhudi za wakazi. Kwa hilo umeanza kuvutia mashirika na taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na kazi hii ya kutunza mazingira. Mojawapo ya mashirika haya ni lile la Kenya Forest Services ambalo ndilo linalohusika na utunzaji wa mazingira haya.Mashirika mengine ni kama lile la wanyama pori pamoja na idara ya uvuvi.Hata hivyo mwenyekiti hhuyu anavulia kofia shirika la KWetu Training Centre ambalo lilijitwika jukumu kubwa wakati mradi huu ukianza hadi leo hii. Shirika la Kwetu Training hutoa mafunzo maalum kuhusiana na utunzaji wa mazingira.
“ Haya na mashirika mengine mengi yamekuwa yakifika hapa kutupa ufahamu kuhusu kuyalinda mazingira na kwa juhudi zao tumefaulu na kufika mbali,” akasema.Mwaka jana, shirika la uhifadhi wa misitu nchini lilitoa udhamini wa kifedha katika mradio mzima wa kupanda mikoko katika ufuo huu. Fedha hizo zililipwa kwa kila aliyefika hapa na kushiriki katika upanzi wa mikoko.
Kulingana na mwenyekiti huyu, udhamini huo uliwafanya wakazi wengi kushiriki ambapo zaidi ya miche 30,000 ilipandwa. Hata hivyo Mzee Kokota anaamini bado kuna safari ndefu ya kuhakikisha kwamba miti zaidi ya mikoko inapandwa.
Aidha alisema kwamba kulingana na mipangilio yao, wanapanga kupanda miche milioni moja katika umbali huo wa kilomita kumi mraba ambao unaanzia katika daraja la Mtwapa hadi katika eneo la Mwakirunge.
“Tumeanzia katika daraja la Mtwapa hadi katika eneo la Mwakirunge. Kufikia Mwakirunge tunapanga pia kupanda miche ya mikoko katika maeneo ya Kashani, Mdengerekeni, Guu Ngombe hadi katika eneo la Colorado na Mwakirunge,” akasema. Kutokana na urefu wa eneo lenyewe, afisa huyu alisema kwamba wameamua kuanzisha makundi mengien chini ya mwavuli wa Kidongo Beach Management Unit ili kuendeleza mpango huo. Jambo hili alisema litahakikisha kwamba wanafanikiwa katika kutimiza malengo yao ya kupanda miche milioni moja kufikia mwaka ujao.
Naye afisa wa misitu ambaye anafanya kazi katika eneo hilo Bi Fatuma Ali Mansoor alishukuru mno juhudi ambazo wakazi wamekuwa wakifanya na kusema kwamba hilo ni kwa ajili ya manufaa yao na taifa kwa jumla.
“Tumekuwa tukishirikiana vyema nao kutokana na juhudi zao. Nadhani wanafanya mchango mkubwa katika kuisaidia serikali kulinda mazingira. Hakuna vile tunaweza kuwa kinyume na wao,” akaiambia Taifa Leo wakati wa uzinduzi rasmi wa upanzi wa mikoko.
Naye aliyekuwa mbunge wa Kisauni Anania Mwaboza na ambaye alikuwa miongoni mwa wageni siku hiyo ya upanzi wa miti aliwataka wakazi waitunze miti hiyo kwani ni muhimu sana kwao.
“Lazima tujue kwamba miti ya mikoko ni muhimu sana kwetu na tunafaa tuitunze ili umuhimu wake tuuone kwa mapana zaidi. Hakuna haja ya kukata kiholela miti ya mikoko kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaharibu mazingira,” akasema.
Kisha chifu wa kata ndogo ya Bamburi Jeremia Machache ambaye pia alikuwepo aliwataka wakazi kuitunza mikoko huku akisema kwamba ni miti ambayo inasaidia sana kuwakuza samaki baharini.




No comments:

Post a Comment